NINI HUTOKEA PALE UNAPO UMIZWA NA MAPENZI

chuwaz.com


Maumivu ya moyo, kuupasua moyo vipande vipande au tamathali zozote tunazotumia kujaribu kuelezea tabu tuipatayo, baada ya kukataliwa au kutengana na mtu ambaye bado tunampenda.

Mwandishi Susan Sontag ameandika katika Reborn, "mapenzi yanaumiza. Ni kama kujisalimisha ili kuchunwa ngozi na ikijua wakati wowote mtu huyo anaweza kuondoka na ngozi yako.

Hilo lilithibitika kwa Florence Williams, baada ya uhusiano wa miongo mitatu uliojumuisha ndoa na watoto wawili na mpenzi wake wa tangu ujana; akakutana na barua pepe ya mume wake.

Ulikuwa ujumbe wa mapenzi kwa mwanamke mwingine. Hakuwahi kuvunjika moyo hapo awali lakini ghafla alijua kuwa kutendwa ni jambo la kweli.

"Nilihisi kama moyo wangu umepigwa shoka, kama kiungo kimepotea, nilikuwa nimezama kwenye bahari, katikati ya msitu wa kutisha. Nilijihisi hatarini," aliandika.

"Nilihisi wasiwasi. Nilikosa usingizi. Nilipoteza takribani kilo 20 kwa siku chache."

Alipofanyiwa vipimo, "waligundua kiwango cha sukari kilikuwa chini sana, kongosho liliacha kufanya kazi vizuri baada ya miezi 5 au 6 ya kutengana, walinigundua nina ugonjwa wa kisukari aina ya kwanza."

Kwa kuwa Florence ni mwandishi, uzoefu ulimsukuma kutafuta majibu. Anasema, "kwa sababu nilikuwa na maswali mengi kuhusu kwa nini nilihisi nilivyohisi."

"Nilitaka kuchunguza kwa nini mfumo wangu wa kinga ulikuwa unatii kwa namna fulani hali yangu ya kijamii au kihisia."

Utafiti wa Kisayansi


Ingawa kumekuwa na tafiti nyingi kuhusu jinsi tunavyopendana, sayansi haijatumia muda mwingi kufikia mwisho wa hadithi hiyo.

Lakini kuna vipande kadhaa vya utafiti vinavyoanza kuweka fumbo hilo pamoja.

Steve Cole, profesa wa Sayansi ya tiba, taikolojia, tabia na maumbile katika idara ya tiba ya Chuo Kikuu cha UCLA, Marekani, ambaye amekuwa akitafiti vinasaba kwa miongo kadhaa.

Mwaka 2007, Cole, pamoja na John Cacioppo, profesa wa saikolojia na sayansi ya tabia kutoka Chuo Kikuu cha Chicago, miongoni mwa wengine, waligundua uhusiano kati ya upweke na vinasaba.

Cole anasema, “upweke ni mojawapo ya jambo baya sana. Unapotokea unaweza kudhuru afya yetu ya mwili na kiakili.”

Katika uchunguzi, Florence alifanyiwa majaribio na Cole, kwa kutumia sampuli ya damu yake. Walipima seli fulani katika mfumo wake wa kinga kwa nyakati tofauti baada ya talaka.

Uchunguzi wa Cole ulionyesha kuwa upweke unaleta hatari zaidi ya kupata virusi na huzalisha seli nyingi zinazosababisha maambukizi.

"Inaonekana kwamba tunapoachwa, miili yetu inatafsiri hali hiyo kwamba tumeachwa peke yetu kwenye uwanda, na hivyo seli nyingi za kupambana na hali hiyo huzalishwa.

Kwa hivyo mwitikio wa kinga za mwili, huongeza ulinzi ili kupambana na majeraha ya kimwili, na hupunguza majeraha mengine.

Tunapohisi kuwa tumeachwa peke yetu, tunajihisi tuko karibu kushambuliwa. Kwa hivyo tunazalisha jeni fulani. Ndio maana watu wapweke wapo hatarini kupata shida ya akili, ugonjwa wa moyo na mishipa na magonjwa mengine sugu.

Hali ya Florence kwa sasa


Mojawapo ya mambo ya kuvutia zaidi, anasema, tunapopendana, shughuli katika sehemu ya ubongo inayozalisha homoni za msongo wa mawazo huongezeka.

Ni kana kwamba tangu mwanzo zilikuwa zikijiandaa kwa ajili ya mwisho. Ndiposa mwenza anapoondoka, uchungu unatuchochea kwenda kumtafuta au tunashukuru sana anaporudi.

Watafiti wengine wamegundua kuwa maumivu na mshtuko wa moyo huchakatwa karibu na sehemu ya ubongo ambayo hushughulika na maumivu ya kimwili. Hilo linaonyesha maumivu ya kihisia huchukuliwa kwa uzito sana katika ubongo wetu kama maumivu ya mwili.

"Sikupenda kusikia kwamba watu wanaoachana wako katika hatari kubwa ya kupata magonjwa sugu na kifo cha mapema, lakini wakati huo huo, nilipata faraja kujua kwamba hii ndio njia ambayo miili yetu hufanya kazi, na wengi wetu tunateseka namna hii,” anasema Florence.

Florence hakuwa na uhakika, alipoanza utafiti wake, kama naye atakuwa miongoni mwa watu 15% ambao hawaponi kabisa baada ya kutengana.

Lakini "sasa niko vizuri sana," anasema.

"Jambo kubwa ni kuelewa kuwa, ikiwa miili hupata maumivu ya kihisia ya kuachwa – pia kuna kupona. Na njia moja ya kupona ni kuwa mkweli kuhusu maumivu yako.

Kwake, njia bora ilikuwa ni kukaa karibu na maumbile ya asili. Alibaini dawa ya upweke sio tu kuwa pamoja na watu, bali pia kukaa karibu na ulimwengu na uzuri wake.

Chanzo 

BBC Swahili

Previous Post Next Post

No Thumbnail

News app yako bomba sasa unaweza idownload kwa kubonyeza batani ya download hapa ,